Thursday, 27 March 2008

zanzibar tuwe kama Arsenal



Arsenal walimu wazuri



ILIKUWA Machi 4, 2008 wakati vijana wadogo kiumri na wanaoonekana kutokuwa wazoefu wa mikiki mikiki mikubwa ya soka la mashindano makubwa, Arsenal kutoka London walipofanya jambo ambalo halikutarajiwa na wengi.

Vijana hao waliivua ubingwa wa Ulaya timu kubwa na maarufu duniani ya AC Milan ya Italia iliyojaa wachezaji maarufu sana, wenye uzoefu sana na waliowahi kupata mafanikio makubwa sana ya soka Ulaya na duniani kwa ujumla.




ADEBAYOR na Fabregas wakishangilia goli

Cha kusisimua ni kwamba vijana hao wa London walifanya jambo hilo kubwa kwa mabao 2-0 ya Cesc Fabregas na Emmanuel Adebayor walioupata kwenye uwanja wa San Siro wa wakali hao wa Italia.

Kabla ya siku hiyo hakuna timu yoyote ya Uingereza iliyoweza kuishinda timu hiyo ya Italia kwenye uwanja huo.

Ukiitazama kwa makini mipango ya timu ya Arsenal na ushindi walioupata dhidi ya AC Milan ugenini baada ya kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyopigwa kwenye Uwanja wao wa Emirates jijini London wiki mbili zilizotangulia, utapata mafunzo yafuatayo:-

Mpira wa miguu ni mchezo wa vijana wadogo Ukiiangalia orodha ya wachezaji wa Arsenal "waliouangusha mbuyu" San Siro, utabaini kwamba wastani wa umri wao ni miaka kama 22 hivi ambapo wastani wa umri wa wachezaji wa AC Milan unakaribia miaka 30.

Wastani wa umri wa wachezaji wa Arsenal ungekuwa mdogo zaidi wasingekuwapo kina kipa Almunia, nahodha Gallas na Gilberto Silva aliyeingia dakika za mwisho.

Kwa upande mwingine, wastani wa umri wa wachezaji wa AC Milan ungekuwa mkubwa zaidi kama wasingecheza kina Pato na Kaka.

Katika hali hiyo, ni wazi wachezaji wa Arsenal walikuwa na pumzi zaidi kuliko wa AC Milan. Isingekuwa ajabu kwao kushinda hata kwa mabao 3-0 kwenye dakika za nyongeza kama AC Milan wangebana hadi pambano kufika dakika 90 likiwa suluhu.

Ni wazi wakati huo AC Milan wangekuwa wamekwisha kabisa kipumzi. Kwa hiyo funzo la kwanza tunalolipata kutoka kwa Arsenal ni kwamba soka ni mchezo wa mafanikio kwa timu yenye vijana wadogo wengi.

La msingi ni kuwa na vijana wadogo wenye vipaji na kuwapa maandalizi mazuri.

Tuwaamini wachezaji wa soka wenye umri mdogo.

Funzo la pili tunalojifunza kutoka kwa Arsenal ni kuwaamini wachezaji wadogo. Kwa kufanya hivyo, wachezaji hao wanajenga moyo wa kujiamini na wanafanya juhudi kutopoteza imani hiyo waliyopewa.

Mwaka jana, vijana wadogo tupu wa Arsenal ambao sasa ndiyo timu yenyewe ya kikosi cha kwanza waliaminiwa kucheza mashindano ya Kombe la Ligi (Carling Cup) hadi kuifikisha timu fainali.





KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger

Walipofika fainali, walikumbana na timu kubwa na ngumu ya Chelsea. Wengi waliamini kocha wao Arsene Wenger angebadili kikosi hicho lakini alichezesha hicho hicho cha vijana wadogo bila kujali kukosa taji ambalo msimu huo lingekuwa pekee. Walifungwa mabao 2-1 lakini mechi hiyo iliwaongezea kujiamini baada ya kuona wameaminiwa.

Katika kuwaamini wachezaji wake chipukizi, Wenger, hawatelekezi wanapoharibu mechi bali huzidi kuwatumia kuwajengea hali ya kujiamini.

Kwa mfano, miezi ya kati kati ilionekana kijana mdogo sana Theo Walcott alikuwa anashindwa kutoa mchango wa maana kwa timu na baadhi ya watu kushauri kijana huyo auzwe kwa mkopo, jambo ambalo Wenger amelikataa na kuendelea kumuamini.

Matokeo ya kumuamini huko, ni kijana huyo aliyetia krosi iliyopigwa kichwa na Adebayor kilichogonga mwamba kwenye dakika za mwisho za mchezo wa kwanza wa Arsenal na AC Milan.

Aidha, ni kijana huyo mdogo, anayezidiwa miaka 21 na Paolo Maldini wa AC Milan, aliyeruka kwanja kwenye dakika za mwisho kabisa za mechi ya marudiano, kukata mbuga hadi kuingia ndani ya eneo la mita 18 la AC Milan na kutoa pasi kwa Adebayor ya kumuwezesha kufunga kirahisi bao la pili.

Mtoto huyo aliyafanya hayo siku si nyingi baada ya kufunga mabao yote mawili ya Arsenal ilipotoka sare ya 2-2 nyumbani kwa Birmingham City katika Ligi kuu ya England.

Makali yake ya sasa, ambayo ni wazi yataongezeka, ni matokeo ya yeye kuaminiwa kama wanavyoaminiwa wenzake wanaochezea timu hiyo.

Kwenye mashindano, timu zote zina nafasi sawa Kutokana na matokeo ya AC Milan dhidi ya Arsenal tumejifunza pia kwamba timu zinapokuwa mashindanoni kila moja ina nafasi sawa ya kushinda.

Wengi waliokuwa wanaisubiri mechi ya AC Milan na Arsenal hawakutarajia kama Arsenal ingeweza kupata ushindi mkubwa hivyo ugenini lakini Arsenal walishinda.

Timu zetu nazo zijenge utamaduni wa kuamini kuwa zikijipanga vizuri zinaweza kuishinda na kuitupa nje ya mashindano timu yoyote watakayokutana nayo katika mashindano ya vilabu barani Afrika.

Hali ya kujiona wanyonge baada ya kujua watapambana na nani, huzifanya timu zetu zitolewe kabla ya mechi.

Hii si kwa vilabu tu, hata kwa timu ya taifa. Naamini tungekuwa na ujasiri wa Arsenal, mwaka jana Senegal wangeambulia kutoka kwetu, sana sana, pointi moja ya mchezo wa kwao.

Kwa bahati mbaya tulitishwa na jina bila kujua kuwa Senegal hii si ile ya miaka ya nyuma kama ilivyodhihirika kwenye fainali za Ghana. Basi tuwe Arsenal wakati tutakapocheza na Cameroun mwaka huu.

Ushindi hupatikana popote

Jambo la mwisho walilotufundisha Arsenal kwa kuitoa mashindanoni AC Milan ni kwamba ushindi hupatikana popote pale. Hapa kwetu tuna lugha ya ajabu na ya kinyonge. Wawakilishi wetu wanapocheza nyumbani na timu kali kama Al Ahli ya Misri au Esperance ya Tunisia,wanaposhinda kwa bao 1-0, tunasema wamefanya kosa kubwa kwa kushindwa kufunga mabao mengi kama 3-0 au zaidi na hivyo kujiweka katika mazingira magumu kwenye mechi ya marudiano!

Al Ahli ni ndogo kiasi gani mpaka tuipigie hesabu ya mabao 4-0? Hilo 1-0 lenyewe tu, kulipata tunapaswa kushukuru.

Kutokana na kauli hizo, timu yetu inayoshinda hapa kwa ushindi mwembamba, inaenda kwenye mechi ya marudiano ikijihesabu imetolewa tayari! Tujenge utamaduni wa kuamini kuwa ushindi hupatikana popote.

Tunashinda hapa 1-0, tunashinda tena ugenini. Mfano mzuri wa miaka ya karibuni ni wa Yanga. Ilitoka sare ya 2-2 na Highlanders ya Zimbabwe hapa nyumbani lakini ikaenda kushinda 2-0 ugenini kwa mabao ya Ally Yussuf Tigana.

Arsena ni walimu wazuri kwetu. Naomba tulielewe vizuri somo lao kwa mafanikio yetu.

No comments: