Sunday, 23 March 2008
Abdi kassim pele wa Zenj
Babi` wa Yanga mwenye mashuti yanayomkuna Maximo Stars
Licha ya kukiri kwamba wapinzani wao katika ligi kuu ndogo ya Bara inayoendelea sasa kwa mtindo wa makundi ni wagumu, kiungo mshambuliaji Abdi Kassim `Babi` wa Yanga amesema klabu yake itafanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa inaoushikilia kwa mwaka wa pili sasa.
`Babi` ameiambia Lete RAHA mwishoni mwa wiki kuwa kikosi chao kiko safi na kwa sababu hiyo, hakitababaishwa na changamoto za wapinzani katika kutwaa tena ubingwa wa Bara na hatimaye kuwakilisha tena nchi katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kama ilivyokuwa mwaka huu na mwaka jana.
``Nini? ubingwa? Mie sikuwepo mwaka juzi ulipochukuliwa na Yanga wala mwaka jana. Lakini naamini tutafanya vizuri kama miaka hiyo,`` anasema Kassim, kiungo ambaye pia ni miongoni mwa wanaounda kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
MASHUTI YA MBALI
Tangu alipokuwa na `Wakata Miwa` Mtibwa wa Turiani Morogoro, Kassim alikuwa mwiba mchungu kwa maadui.
Mara zote alifahamika kwa staili yake ya kucheza kwa utulivu, akimiliki mpira kwa namna iliyomfanya awe na namba ya kudumu katika kikosi cha timu hiyo inayomilikiwa na Kiwanda cha Sukari na pia akifunga mabao mazuri yaliyoifaidisha timu yake hiyo.
Kwa umahiri wake, akajikuta akiitwa mfululizo kwenye vikosi vya timu ya taifa ya Zanzibar, Mapinduzi Stars, na pia timu ya Taifa, Taifa Stars.
Na alipotua Yanga msimu huu, Kassim akaendeleza mambo yake.
Hadi sasa amekuwa miongoni mwa wachezaji waliokubaliwa mapema uwezo wao na kocha Milutin Sredojevic `Micho` na pia mashabiki wa timu hiyo.
Staili yake ya kupiga chenga muhimu, kutoa vyumba safi na mashuti yake ya kustukiza imeendelea kumuweka katika kundi la wachezaji `nyota` wa timu hiyo.
Kocha Marcio Maximo wa Taifa Stars amekuwa akivutiwa na vitu vyake `adimu`, hasa mashuti yake ya mbali ambayo mara kadhaa huleta kashakash za mabao langoni mwa maadui.
Katika moja ya vitu vyake adimu, Kassim alitoa mchango mkubwa katika `kuwaonea` Wacomoro AGSM kwa kuwapiga mabao 5-1, huku yeye akitengeneza la tatu kutokana na pasi yake ndefu kumkuta Maulid `SMG` aliyekuwa katika nafasi nzuri na kufunga.
Na katika safari yao hiyo ya kuelekea kwenye hatua ya timu 16 bora za Ligi ya Klabu Bingwa Afrika iliyoishia ukingoni mwa Esperance ya Tuniasia, Kassim alifunika mno siku walipocheza na Waangola Petro Atletico nyumbani na kushinda 3-0.
Ni siku hiyo vilevile, jina lake la utani la \'Babi\' lilipopata nguvu zaidi midomoni mwa wana Yanga.
`BABI`?
Siku hiyo na Waangola Atletico, Kassim aling\'ara kwelikweli. Licha ya kwamba jamaa walikuwa wagumu kufungika, Kassim alifanya anavyotaka katikati ya uwanja. Alikimbiza kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho. Aliweza kuwa nyota wa mchezo wa siku hiyo.
Kutokana na `presha` zake, Mwaikimba na wengine, wakapata bao la kwanza mnamo dakika ya 77 baada ya wageni kujifunga.
Dakika tano baadaye, Kassim alipata mpira akiwa mbali na lango la maadui.
Akaujaza vyema mguuni mwake na kufumua shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuzaa bao `tamu` la pili.
Baada ya hapo, shangilia yake ya kama anabembeleza mtoto mchanga ikawapagawisha mashabiki waliofurika Uwanja wa Taifa ili kuishangilia timu yake. Jina la`Babi`, kwa maana ya Baby, likawa limeshika.
Hivi sasa Kassim anatarajiwa kushirikiana na `wakali` wenzie kibao Yanga ili kufanya vizuri kwenye kundi `B` la ligi kuu ndogo ya Bara kituo cha Arusha na katika maandalizi kuing`oa El-Mereikh ya Sudan katika raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment