Saturday, 29 March 2008
machupa na gabriel hamna wiva
uvumi uliosikika siku za nyuma kwamba washambuliaji wawili mahiri wa Simba, Emmanuel Gabriel na Athuman Machuppa hawaivi vizuri kwa sababu ambazo haziko wazi.
Wakati mwingine hakuna unachoweza kutegemea kutoka kwa washambuliaji wawili wa Kitanzania wanaong’ara pamoja zaidi ya hisia za wivu na hata kurogana
Labda wana hisia kwamba hawawezi kucheza pamoja uwanjani na kila mmoja wao akang’ara. Labda wana hisia kwamba mmoja anamzibia mwenzake nyota yake kung’ara.
Lakini laiti kama ningekuwa mshauri wa Machuppa au Gabriel, kitu kimoja ningewaambia kwa uwazi zaidi kwamba hakuna sababu ya kuoneana wivu wala kurogana.
Kama wote wawili wakizifanya kazi zao kwa ufasaha, kila mmoja anaweza kung’ara uwanjani bila ya kumhofia mwenzie. Na zaidi, kuna uwezekano mkubwa kuwepo kwa wote wawili uwanjani kukawafanya wawe mahiri zaidi pengine kuliko inavyokuwa pale mmoja wao anapokaa nje ya uwanja.
Kwa nini? Kwa sababu hawa ni washambuliaji wawili tofauti ambao kocha yeyote wa soka anaweza kuwatumia uwanjani kutokana na utofauti wa staili zao.
Kwa Gabriel, huyu ni mfungaji asilia ambaye ana uwezo mkubwa wa kuwa kidokozi katika eneo la hatari la adui. Kwa wazungu washambuliaji wa aina hii huwa wanaitwa fox in the box au goal getter
Na hata mchambuzi wa soka, mlinzi mahiri wa zamani wa Manchester United, Paul Parker alipata hisia hizo wakati alipokuwa akichambua mechi kati ya Simba na Prisons iliyoonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha kulipia cha GTV ambako Gabriel alifunga mabao matatu (hat trick)
Ukimtazama Gabriel ni wazi kwamba hana ubora mwingi akiwa mbali na eneo la hatari. Hana kasi wala uwezo mkubwa wa kutambuka walinzi na kwenda zake kupachika bao.
Ubora wake mkubwa uko katika kupachika mabao akiwa karibu na eneo la hatari. Na huu si ujinga bali ni kipaji cha hali ya juu kwa sababu si kila mchezaji ana uwezo mkubwa wa kujiweka katika maeneo ya hatari na kufunga.
Baada ya ushuhuda wa kuondoka kwa Zamoyoni Mogella ‘original’ wa miaka ya 1980, halafu akaja Mohamed Hussein wa miaka 1990 na kisha akaondoka zake, walau unaweza kusema Gabriel ndiye ‘shetani’ wa eneo la hatari aliyefuatia katika miaka ya 2000
Mchezo wa wachezaji wa aina hii unahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wachezaji wa nafasi za viungo wa ushambuliaji, mshambuliaji anayecheza nyuma yake (playmaker) au pia mawinga wa pembeni.
Ukitazama namna Gabriel alivyoikimbilia nafasi yake katika pambano la Ashanti wakati akisubiri krosi ya Ramadhan Wasso, ni wazi mtazamaji angejua kwamba kilichofuata kingekuwa bao.
Wakati Wasso akikimbizana na mpira katika upande wa kushoto, Gabriel alikuwa bize akijitafutia nafasi ya karibu kabisa na lango huku walinzi wa Ashanti na baadhi ya washambuliaji wa Simba wakitegea.
Krosi ilipompita kipa wa Ashanti ilitua katika kichwa chake. Hakuhitaji kuupiga kichwa mpira ule zaidi ya kuegesha tu mpira ugonge kichwa.
Huyu ndiye Gabriel, lakini jaribu kumtazama Machuppa. Ana staili tofauti ya uchezaji na ana tofauti kubwa na Gabriel.
Machuppa ana uwezo mkubwa wa kushambulia akiwa mbali na lango. Kasi yake ya mchezo ni kubwa na hasa wakati ule alipokuwa mchezaji chipukizi. Bahati nzuri, ana ‘jicho’ zuri afikapo langoni mwa adui.
Unaweza kutumia neno ‘bahati’ kwa sababu ni washambuliaji wachache wenye kasi na uwezo wa kutambuka mabeki ambao wana shabaha nzuri ya kufunga.
Washambuliaji wengi wenye kasi za marathon au uwezo wa kuwatoka walinzi, hawana shabaha kubwa katika ufungaji kuliko wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa kipawa cha kuvizia kama Gabriel.
Ukichunguza kwa mifano ya Ulaya, japo wachezaji wetu hawajaweza walau kunusa ubora wa kufananishwa na wachezaji wa Ulaya, unaweza kuifananisha hali hii kwa kuwatazama washambuliaji Thierry Henry wa Barcelona na Ruud Van Nisterlooy wa Manchester United.
Hawa tunawafahamu kwa sababu tuliwatazama kwa kipindi kirefu katika ile ligi iliyozoeleka zaidi Tanzania yaani Ligi Kuu ya England.
Henry pamoja na kasi yake na ubora wake mwingi, lakini ni wazi kwamba hakuwa na shabaha kali ya lango kama ilivyo kwa Van Nisterlooy. Kinyume chake ni hivyo hivyo, Van Nisterlooy pamoja na shabaha yake kali langoni, lakini hakuwa msumbufu kwa walinzi
Je watu wa aina hii hawawezi kucheza pamoja? Je Machuppa na Gabriel hawawezi kucheza pamoja? Jibu ni hapana. Watu hawa wanaweza kucheza tena kwa ufanisi mkubwa.
Katika mifumo ya kisasa mmoja anaweza kucheza mbele na mwingine akacheza nyuma yake. Na kwa kuwatazama wote wawili, Machuppa, kutokana na kuwa na kasi kubwa, ana uwezo wa kurudi mpaka katikati ya uwanja na kuchukua mipira kwa watu wa nafasi ya kiungo.
Kwa kasi yake anapaswa kuwa na visheni kubwa ya kupiga pasi za mwisho kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuwatoka walinzi na kutengeneza nafasi kwa wengine.
Kufunga ni majaliwa, lakini kitu kikubwa ni kwamba unapokuwa na uwezo wa aina hii, unapata fursa kubwa ya kutengeneza mabao kwa wengine. Na ndio maana ulitokea msimu ambao Henry alifanikiwa kupiga pasi za mwisho 24 na kuvunja rekodi za pasi za mwisho zilizozaa mabao katika Ligi Kuu ya England.
Kwa Gabriel anaweza kunufaika na kasi ya Machuppa kwa kufungua nafasi za kufunga kwa sababu kuna ukweli kwamba walinzi wanahangaika zaidi na mchezaji aliye na mpira na mwenye kasi kuliko ambaye amejificha nyuma ya kivuli akifungua nafasi.
Bahati mbaya kuna walinzi ambao siku zote wanahaingaika na mchezaji anayefungua zaidi nafasi kuliko mwenye mpira. Hali hii iliwakuta walinzi wa Arsenal katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA uwanja wa Villa Park mwaka 1999.
Walinzi wa timu hiyo walijishughulisha zaidi na wachezaji wa Manchester United waliokuwa wamefungua nafasi, kuliko Ryan Giggs aliyekuwa na mpira. Waliposhtuka Giggs alikuwa anaingia katika eneo lao la hatari na hatimaye kumtungua kipa David Seaman.
Kwa mtindo kama huu, Machuppa na Gabriel wanaweza kutumiana kwa njia moja au nyingine katika kupasiana au kufunguliana nafasi. Na bahati nzuri, kila mmoja ni bora katika aina tofauti ya mchezo anayotumia.
Hii lugha ya ‘kurogana’ ingeweza kuvuma au kueleweka kama wachezaji hawa wangekuwa Mohamed Hussein na Gabriel. Wote hawa ni wachezaji wa aina moja na walau wangeweza kuzibiana bahati.
Ni wazi kwamba kama Gabriel na Machuppa hawapendani au ‘wanarogana’ kama tunavyoelezwa basi ni kwa sababu ya kuogopa vivuli vyao au kutojiamini katika uwezo wa vipaji vyao tofauti.
Kama kila mmoja akiifanya kazi yake kwa ufasaha ni wazi kwamba wana uwezo wa kucheza pamoja na kuwa mahiri kwa pamoja. Tatizo ni lile lile la wachezaji wetu kutojiamini na kufikiria kwamba Simba na Yanga wamefika.
Na hata ukimlazimisha Gabriel acheze mpira wa Machupa hawezi kufanya hivyo, na ukimlazimisha Machupa acheze katika staili ya Gabriel utakuwa unalazimisha vitu visivyowezekana. Ni kulazimisha vitu visivyowezekana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment