Monday, 24 March 2008

simba taabani


Enyimba yaimaliza Simba

2008-03-24 09:50:11
By Mwandishi Wetu


Simba jana ilidhihirisha bado haijapata dawa ya kuifunga Enyimba ya Nigeria baada ya kuchakazwa 4-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika uliofanyika mkatika uwanja wa Enyimba mjini Aba.

Matokeo hayo ni marudio ya mwaka 2004, ambapo Simba ilichakazwa 4-0 katika mechi ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Mwanza.

Simba pia ilipata kuchapwa 3-0 mjini Aba mwaka 2003 wakati timu hizo zilipokutana kwenye mechi ya makundi, hata hivyo, Simba ilikuwa imeifunga Enyimba 2-1 katika mchezo mwingine wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kwa matokeo hayo, Simba ina kazi ya ziada ya kushinda 5-0 ili kusonga mbele kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa baada ya wiki mbili.

Timu hiyo, hata hivyo, ilipokea na kipigo hicho na kibaya zaidi kwa muda mrefu ililazimika kucheza na watu 10 baada ya kutolewa kwa kiungo wake tegemeo, Henry Joseph katika dakika ya 37.

Katika mchezo huo, ambao mwamuzi William Agogo alionekana wazi kutoa maamuzi mengi ya kutatanisha na alimtoa Joseph kwa madai ya kumchezea vibaya mshambuliaji hatari wa Enyimba, Worku Stephen.

Katika mchezo huo, ulioanza saa 10 za jioni kwa saa za Nigeria (saa 12 kwa saa za Tanzania), wenyeji walionyesha hawakuwa na mzaha wakati walipoweza kupata bao la kuongoza katika dakika ya saba tu.

Worku aliweza kuzamisha bao hilo baada ya mabeki wa Simba kuzubaa kumzuia wakidhani alikuwa ameotea.

Bao hilo lilifanya Simba wacharuke na mshambuliaji wa Simba, Athumani Machupa alipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha katika dakika ya 26.

Enyimba, hata hivyo, iliweza `kuzawadiwa` na Kipa wa Simba, Juma Kaseja katika dakika ya 36.

Kaseja alipiga mpira kwa nia ya kwenda kwa mmoja wachezaji wake na Worku aliweza kuwahi na kupiga shuti kali lililopita kushoto kwa Kipa Kaseja.

Hata hivyo, baada ya moja dakika tu, Simba ilipata pigo baada ya kutolewa kwa Henry.

Lilikuwa pigo kwa Simba na ikalazimika sasa kucheza kwa muda mwingi kwa kujihami na kuweza kutoa mwanya kwa Enyimba kuishambulia vikali.

Pamoja na mashambulizi huyo ya Enyimba na pia mwamuzi Agogo naye alionekana wazi kutoa maamuzi ya kusaidia Enyimba.

Mathalani alipuuzia kuumizwa kwa Emmanuel Gabriel, ambapo alitibiwa kwa muda mrefu nje ya uwanja.

Mwamuzi huyo baadae alitoa penati kwa Enyimba baada ya Nico Nyagawa kucheza rafu ndani ya eneo la hatari.

Worku aliweza kuzamisha penati hiyo katika dakika ya 76 baada ya kupiga shuti kali lililopita kulia kwa Kaseja.

Baada ya hapo Simba ilionekana wazi kukata tamaa na Enyimba ikamalizia mauaji yake baada ya kupata penati nyingine katika dakika ya 88 iliyofungwa na Kali Uche.

Simba iliwakilishwa na:Juma Kaseja, Nicodemus Nyagawa, Nurdin Bakari, Kelvin Yondani, Henry Joseph, Mohamed Banka, Mussa Hassan `Mgosi`, Mohamed Kijuso (Juma Nyosso), Athumani Machupa (Joseph Kaniki), Emmanuel Gabriel na Ulimboka Mwakingwe.


SOURCE: Nipashe

No comments: