Thursday, 27 March 2008
kaka ,ronaldo, messi nani tishio la ulaya?
Kaka, Ronaldo, Messi: Katika kilinge cha ufalme wa kulichezea gozi duniani champion
Tuzo hiyo ambayo hutolewa na Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), itatolewa katika Makao Makuu ya Shirikisho hilo kwenye ukumbi wa Opera House jijini Zurich nchini Uswisi Jumatatu ya Desemba 17 mwaka huu.
Mshindi wa Kombe la Ligi ya mabingwa Ulaya akiwa na AC Milan, Kaka, hana cha kupoteza katika tuzo hiyo kutokana na kuwa na kiwango bora zaidi kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, lakini hicho si kigezo cha kuwabeza washindani wake Ronaldo na Messi.
Ronaldo ametwaa tuzo karibu zote za soka katika ardhi ya nyumbani kwake Ureno na Uingereza anakocheza soka la kulipwa, huku akiifikia rekodi ya mchezaji wa zamani wa Aston Villa na Scotland, Andy Gray aliyoiweka mwaka 1977 ya kutwaa tuzo ya mwansoka bora wa mwaka wa PFA na mchezaji bora chipukizi wa mwaka ndani ya msimu mmoja.
Messi amezidi kuwa na wakati mzuri zaidi katika kikosi chake cha Barcelona na Timu ya Taifa ya Argentina. Ingawa timu yake ilishindwa kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya na la lile la Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita, haitakuwa sababu ya kumzuia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 kutajwa katika tuzo hizo.
Kaka:
Brazil ni sehemu inayozalisha vipaji vingi vya soka duniani. Wengi wakifuata nyao za wachezaji kama Romario, Rivaldo, Ronaldo, Ronaldinho na Ricardo Izecson Santos Leite.
Kaka, anajulikana kwa mashabiki wengi wa soka kutokana na uwezo wake dimbani, kumiliki mpira, kupiga chenga, kutengeza pasi nzuri za kuzaa magoli na maamuzi yake ya haraka anapokuwa na adui, hizo ni baadhi ya sehemu zinazong’arisha kipaji chake.
Historia ya Kaka kuelekea kilele cha mafanikio katika usakataji wa soka ni ya kuvutia. Alikulia katika familia ya maisha ya kati iliyomuwezesha kupata elimu kiurahisi na mahitaji yake yote ya muhimu.
Wakati baba yake Bosco ni Muhandisi kitaaluma, lakini amekuwa akimfuatilia mwanawe na kumsimamia katika kila mkataba ambao anakuwa akiingia kwenye soka.
Akiwa amezaliwa katika mji Mkuu wa Brazil, Brasilia mwaka 1982, Kaka alikulia katika jiji la Sao Paulo baada ya wazazi wake kuhamia huko wakati akiwa na umri wa miaka saba.
Kama ilivyo kwa ndoto za watoto wengi wa umri wake, alipenda kucheza soka kama sehemu ya kujiburudisha kabla ya kuanza kuitilia mkazo alipofikisha umri wa miaka 15.
Hata hivyo, akiwa na umri wa miaka 18, nusura ndoto yake ya kuendelea kucheza soka la kulipwa iyeyuke baada ya kupata ajali iliyomsababisha kuumia mbavu wakati anaogelea kwenye ‘swimming pool’: “Baada ya kupona hakika nilikubali kwamba ni mkono wa Mungu ndiyo ulioniokoa,” ameandika katika kitabu cha maisha yake.
Safari ya Kaka katika maisha ya soka haikuwa na milima na mabonde, kwani ilinyoka. Mwaka 2001, alijikuta yupo katika kikosi cha timu ya vijana cha Sao Paulo. Haraka sana ndani ya umri wake huyo wa miaka 18 tayari ‘alibebwa’ na kuingizwa katika timu ya wakubwa na Januari 31, 2002, aliichezea Timu yake ya Taifa ya Brazil kwa mara ya kwanza dhidi ya Bolivia. Na tangu hapo hakuna kilichomzuia kuelekea kilele cha mafanikio ya usakataji wa soka.
Miaka mitatu baadaye, nyota wa zamani wa timu ya Sao Paulo na AC Milan, Leonardo, ambaye amekuwa akifutilia maendelea ya kipaji cha Kaka kwa karibu zaidi, alimshawishi yeye na familia yake kutafuta timu nchini Italia, kitu alichokubali na kukitekeleza kwa kujiunga na AC Milan wakati wa majira ya joto mwaka 2003.
Katika soka la Ulaya mambo yamezidi kumuendea viuri zaidi, kwani msimu wa mwaka 2003/04 aliisaidia timu yake kutwaa taji la 17 la Ligi Kuu ya Italia, Serie A.
Msimu uliopita alikisaidia kikosi hicho cha Rossoneri kutwaa taji la Ligi ya mabingwa Ulaya, huku yeye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo akiwa ametikisa nyavu mara 10.
Messi:
Kwa miaka kadhaa saa katika soka la Argentina, mashabiki wamekuwa wakimheshimu kama Diego Maradona.
Mara nyingi amekuwa akikataa na kujiona kwamba bado hajaweza kufikia mafanikio ya Maradona, lakini winga huyo wa Barcelona anayetumia guu la kushoto kutikisa nyavu za goli lolote analolishambulia, alifanya kile alichokifanya El Diego, wakati alipofunga bao dhidi ya timu ya Getafe Aprili mwaka huu.
Alifunga bao la ‘Mkono wa Mungu’ kama alilofunga Maradona akiwa na jezi namba 10 wakati wa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986 dhidi ya Uingereza.
Katika hafla fulani Maradona mwenyewe aliwahi kusema: “Sasa nimemuona mchezaji atakayechukua nafasi yangu katika soka la Argentina na huyo si mwingine bali ni Lionel Messi.”
Akiwa amezaliwa Juni 24 mwaka 1987 jijini Rosario, Santa Fe, Messi amekuwa chachu kubwa ya vijana wengi hivi sasa kujikita katika soka nchini kwake Argentina.
Akiwa na umri wa miaka 13, kutokana na matatizo ya kiuchumu nchini Argentina, aliamua kuhamia Hispania akiwa pamoja na familia yake.
Baada ya kuonyesha kipaji cha hali ya juu wakati akicheza na watoto wenzake katika mitaa ya Barcelona, hatimaye alialikwa katika Dimba la Camp Nou kwa ajili ya majaribio, na kusajiliwa moja kwa moja huku akianza kucheza Ligi ya Hispania kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Bao lake la kwanza alifunga Mei mosi dhidi ya Albacete, na hivyo kuweka historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungua timu hiyo goli katika Ligi Kuu, ambapo aliivunja rekodi iliyowekwa na Bojan Krkic miaka kadhaa iliyopita.
Mapenzi yake na rangi za blue na nyeupe za Timu ya Taifa ya Argentina yalianza miezi kadhaa baadaye baada ya kuwa stelingi katika Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 akiongoza kuifunga Uholazi kwenye Fainali za Kombe la Dunia la U-20 mwaka 2005 ambapo aliibuka na kiatu cha dhahabu baada ya kuwa mfungaji bora.
Agosti mwaka 2004, kocha Jose Nestor Pekerman alimpanga kwa mara ya kwanza Messi kucheza katika kikosi cha Argentina dakika zote 90 kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Hungary.
Ronaldo:
Cristiano Ronaldo Santos Aveiro hakuna shaka kwamba ni moja ya kipaji cha soka kilicho juu zaidi katika ulimwengu wa soka hivi sasa.
Uwezo wake wa kupiga chenga zenye maudhi huku akikimbia kwa kasi ya ajabu akiwa na mpira ni moja ya vitu vilivyowafanya baadhi ya mashabiki kumfananisha na wajina wake Ronaldo Luis Nazario de Lima kutoka Brazil.
Akiwa amezaliwa kwenye Kisiwa cha Madeira Februari tano mwaka 1985 nchini Ureno, alianza safari yake ya soka la kulipwa akiwa na timu ya Nacional kabla ya mwaka 2002 kuhamia kwa miamba ya jiji la Lisbon, Sporting, akiwa na umri wa miaka 17.
Tangua hapo hakuna kilichomzuia kuendeleza kipaji chake katika ulimwengu wa soka la kimataifa. Wakati wa msimu wake huo mmoja akiwa na klabu hiyo alicheza mechi 25 na kufunga mabao matatu.
Wakati mzuri zaidi kwa kipaji cha Cristiano Ronaldo, ni kipindi ambacho Manchester United ilipoomba mechi ya kirafiki dhidi ya Sporting mwaka 2003, wakati ikiwa katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza. Uwezo wake aliouonesha katika mchezo huo ambao Wareno hao walishinda mabao 3-1, kilikuwa kishawishi tosha kwa kocha wa Mashetani Wekundu hao, Sir Alex Ferguson kuamua kumsajili kwa dau kubwa.
Tangu amejiunga na Manchester amekuwa na wakati mzuri wa kufurahia kipaji chake cha soka katika kila sekunde.
Ifuatayo ni orodha ya wanasoka waliowahi kutwaa tuzo ya mwaka soka bora wa dunia, nafasi ya kwanza hadi ya tatu, tangu ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1991, kwenye mabano ni nchi anayotoka mchezaji.
Mwaka 2006
1. Fabio CANNAVARO (Italia)
2. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
3. RONALDINHO (Brazil)
Mwaka 2005
1. RONALDINHO (Brazil)
2. Frank LAMPARD (Uingereza)
3. Samuel ETO’O (Cameroon)
Mwaka 2004
1. RONALDINHO (Brazil)
2. Thierry HENRY (Ufaransa)
3. Andriy SHEVCHENKO (Ukraine)
Mwaka 2003
1. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
2. Thierry HENRY (Ufaransa)
3. RONALDO (Brazil)
Mwaka 2002
1. RONALDO (Brazil)
2. Oliver KAHN (Ujerumani)
3. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
Mwaka 2001
1. LUIS FIGO (Ureno)
2. David BECKHAM (Uingereza)
3. RAUL (Hispania)
Mwaka 2000
1. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
2. LUIS FIGO (Ureno)
3. RIVALDO (Brazil)
Mwaka 1999
1. RIVALDO (Brazil)
2. David BECKHAM (Uingereza)
3. Gabriel BATISTUTA (Argentina)
Mwaka 1998
1. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
2. RONALDO (Brazil)
3. Davor SUKER (Croatia)
Mwaka 1997
1. RONALDO (Brazil)
2. ROBERTO CARLOS (Brazil)
3. Dennis BERGKAMP (Uholanzi)
3. Zinedine ZIDANE (Ufaransa)
Mwaka 1996
1. RONALDO (Brazil)
2. George WEAH (Liberia)
3. Alan SHEARER (Uingereza)
Mwaka 1995
1. George WEAH (Liberia)
2. Paolo MALDINI (Italia)
3. Juergen KLINSMANN (Ujerumani)
Mwaka 1994
1. ROMARIO (Brazil)
2. Hristo STOICHKOV (Bulgaria)
3. Roberto BAGGIO (Italia)
Mwaka 1993
1. Roberto BAGGIO (Italia)
2. ROMARIO (Brazil)
3. Dennis BERGKAMP (Uholanzi)
Mwaka 1992
1. Marco VAN BASTEN (Uholanzi)
2. Hristo STOICHKOV (Bulgaria)
3. Thomas HAESSLER (Ujerumani)
Mwaka 1991
1. Lothar MATTHAEUS (Ujerumani)
2. Jean-Pierre PAPIN (Ufaransa)
3. Gary LINEKER (Uingereza)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment