Saturday, 29 March 2008
Torres amewaziba midomo Waingereza
Torres amewaziba midomo Waingereza
HAKUNA neno rahisi wanalopachikwa wachezaji wengi mahiri walionunuliwa kwa bei mbaya katika Ligi Kuu ya England kisha wakashindwa kuonyesha makali yao kama neno Flop.
Hili ni neno la kejeli linalomaanisha kushindwa kwa hali ya juu. Ni neno la dharau na chungu miongoni mwa wachezaji wengi wa kigeni wanaotua England na kushindwa kuonyesha makali yao.
Kamuulize mshambuliaji wa Ukraine, Andriy Shevchenko ni neno gani la Kiingereza alilolielewa kwa wepesi mkubwa atakwambia ni neno Flop.
Sababu kubwa ni ukweli kwamba hili ni neno ambalo kila kukicha limekuwa likitumika kama kejeli kwake na magazeti mbalimbali ya Uingereza kama vile The Sun, The Independent, The Guardian na mengineyo.
Kisa ni wivu mkubwa miongoni mwa mashabiki na vyombo vya Habari vya Uingereza pindi mchezaji mahiri kutoka taifa jingine anapotua Uingereza kwa sifa nyingi na kununuliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa wasiowajua Waingereza, kwao ni halali kwa mchezaji wa Kiingereza kununuliwa fedha nyingi, lakini si kwa mchezaji wa nje.
Na ndiyo maana mpaka leo wako kimya na hawataki kuzungumzia ‘upotevu’ wa fedha uliofanywa na Tottenham Hotspurs kumsajili mshambuliaji Darren Bent kwa kiasi cha Pauni milioni 17.
Ndiyo maana mpaka leo wako kimya kuuzungumzia usajili wa Francis Jeffers, ambaye Arsene Wenger alimsajili kwa makeke kutoka Everton kwa uhamisho uliovunja rekodi ya Arsenal wakati huo, Pauni milioni 10, akaishia kucheza mechi 22 tu na kufunga mabao manne.
Wako wachezaji wengi wa aina hii, lakini kwa sababu ni Waingereza, neno la Flop huwa halitumiwi sana. Zinazungumzwa lugha nyingine za kuficha ukali wa dharau.
Lakini kwa Shevchenko kila siku ni kelele. Na si kwa Shevchenko tu, kina Juan Sebastian Veron, Hernan Crespo, Jose Antonio Reyes, Michael Ballack na wengineo wengi walikumbana na neno flop kwa umaarufu mkubwa kuliko wachezaji wengine wa Kiingereza.
Alipowasili Fernando Torres, huku akivunja rekodi ya uhamisho wa klabu kubwa kama Liverpool, kwa kusajili kwa kiasi cha Pauni milioni 21, zaidi ya Sh bilioni 46 za Tanzania, mashabiki wengi wa Kiingereza walikaa mkao wa kula kushuhudia namna ambavyo mshambuliaji huyu angeshindwa kuonyesha makali yake.
Lakini utasema nini kuhusu Torres? Kabla hata Ligi Kuu ya England haijaisha, tayari ameshawaziba midomo mashabiki ambao walikaa mkao wa kula kuukejeli usajili wake kwa kumuita Flop.
Katika mechi 35 alizoichezea Liverpool hadi wakati naandika makala hii, tayari alikuwa ameshafunga mabao 26 katika michuano ambayo Liverpool inashiriki.
Kikubwa zaidi ni katika Ligi Kuu ya England. Tangu kuondoka kwa Michael Owen mwaka 2004, hakukuwepo na mshambuliaji wa Liverpool aliyefanikiwa kufikisha mabao 20 ya ligi kwa msimu mmoja.
Wamepita na wamekuja wengi kabla yake wakiwemo kina Djibril Cisse, Peter Crouch, Dirk Kuyt na wengineo, lakini hawakuweza kufikisha mabao 20 ya ligi kwa msimu.
Kwa Torres, akiwa sambamba na Emmanuel Adebayor wa Arsenal, tayari ana mabao 19. na zikiwa zimebaki mechi tisa kwa timu yake kumaliza ligi, ni nani anayeweza kucheza kamari na kusema Torres hatafunga bao la 20 na zaidi?
Baada ya kuondoka kwa Owen pia, hakukuwepo na mshambuliaji yeyote wa Liverpool ambaye aliweza kufunga mabao 10 mpaka kufikia kipindi cha sikuu ya Krismasi.
Lakini hilo limekuwa jambo dogo kwa Torres. Waingereza wanatakia nini zaidi?
Siku kadhaa zilizopita alifunga mabao matatu matatu (hat trick) katika mechi mbili mfululizo ndani ya uwanja wa Anfield.
Kwanza ilikuwa Februari 23 alipofunga mabao matatu dhidi ya Middlesbrough, halafu akafunga mabao matatu tena katika mechi dhidi ya West Ham Machi 5.
Kwa kufanya hivi, alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Liverpool tangu mwaka 1946 kufunga hat trick mbili mfululizo katika uwanja wa Anfield.
Kabla ya hapo ni mchezaji Jackie Balmer aliyefanya hivyo miaka 62 iliyopita. Waingereza wanataka nini zaidi?
Zaidi ya yote amewapa mashabiki wa Liverpool mdomo wa kusemea ambao mwanzoni hawakuwa nao. Imekuwa lugha rahisi kwa mashabiki wa Manchester United, Arsenal na Chelsea kutambia wachezaji wao.
Kelele za mashabiki wa timu hizi hata wale waliopo Tanzania zilikuwa zinawazungumzia kina Didier Drogba, Thierry Henry, Ruud van Nistelrooy na sasa hivi Emmanuel Adebayor na Cristiano Ronaldo
Liverpool hawakuwa na mdomo wa kusemea kwa sababu mfungaji wao bora alikuwa anatoka katika sehemu ya kiungo, Steven Gerrard. Lakini sasa hawashikiki mitaani kwa sababu wanaye mshambuliaji wa kujivunia, Torres.
Hata hivyo ukiwa mbali Tanzania ni rahisi kudhani kila Muingereza anakenua meno kutokana na mafanikio ya Torres, lakini ukweli hauko hivyo.
Mafanikio ya Torres yanawaumiza kwa upande mmoja. Kwa kiasi fulani yanaendeleza mkondo ule ule wa Ligi Kuu ya England kutawaliwa na wageni kutoka nje.
Kama ungetaka kujua ni kwa namna gani mafanikio hayo yanawaumiza Waingereza, basi ni pale ambapo Torres angeshindwa kung’ara katika msimu wake wa kwanza na kisha akamaliza ligi akiwa amefunga mabao sita tu ya msimu.
Angekejeliwa kwa kila namna na hasa kile kiasi cha fedha ambacho kilitumika kumsajili.
Zaidi ya yote ni ukweli kwamba mashabiki wengi wa Kiingereza walipenda kuona kocha Rafael Benitez wa Liverpool akimrudisha nyumbani kipenzi chao, Owen.
Si kwamba nawachukia Waingereza, hapana, wana wachezaji mahiri. Tatizo kubwa ni namna ambavyo kelele zao za vyombo vya habari zilivyowapandisha wachezaji wao bei kubwa kuliko hali halisi.
Chelsea ilimsajili ‘Muingereza’ Chris Sutton akitokea Blackburn Rovers kwa ada kubwa ya uhamisho wakati huo Pauni milioni 10. Hata hivyo Sutton alifunga bao moja katika mechi 28.
Msimu uliofuata aliuzwa kimya kimya kwenda Celtic kwa uhamisho wa Pauni milioni 6. Hata hivyo hatukusikia kelele nyingi kama ambavyo zimesikika kutokana na kuchemsha kwa Shevchenko.
Anapotokea mchezaji wa aina ya Torres mara nyingi kelele hizi huwa hatuzisikii. Mpaka pale anaposhindwa ndio tunasikia kelele nyingi za kuwakejeli.
Binafsi namtazama Torres kwa jicho tofauti kidogo. Namtazama kwa jicho la kuwaziba midomo mashabiki na vyombo vya habari vya Uingereza ambavyo vinamwaga kejeli kubwa kwa wachezaji wa kigeni waliosajiliwa kwa fedha nyingi pindi wanaposhindwa kuonyesha makali yao.
Wanafanya hivi wakati wachezaji wao wenyewe wa ndani wananunuliwa kwa bei kubwa, lakini wanashindwa kuonyesha makali yoyote ambayo yanaweza kulinganishwa na bei zao kama Torres alivyofanya.
Anachofanya Torres kwa sasa ni kujitafutia usingizi mtamu kwa siku za usoni.
Walau ameweza kupunguza kelele nyingi dirishani kwake ambazo zingekuja kama angefunga mabao sita tu ya msimu kwa uhamisho wake wa Pauni milioni 21.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment