Saturday, 29 March 2008

Tuanzie kwa Fabregas, Mascherano na Ronaldo


Tuanzie kwa Fabregas, Mascherano na Ronaldo



MIAKA michache iliyopita, Cristiano Ronaldo angeweza kuingia uwanjani akiwa mchezaji nadhifu, mwenye sura nzuri na zaidi ya yote, mwenye kipaji kuliko wachezaji wote uwanjani.

Hili la kipaji lilitazamwa zaidi. Angeweza kupiga chenga zake kwa madaha zaidi, akawakimbiza mabeki kwa kadri alivyoweza, akapiga kanzu, tobo na manjonjo mengine kwa madaha, lakini mwishowe asingepiga pasi ya mwisho au kufunga bao.

Katika sehemu nyingi ambazo mashabiki wa soka wanapenda kutazama mipira jijini Dar es Salaam, walipendelea kumuita Ronaldo kazi bure. Huyu hakuwa mchezaji mahiri japokuwa alikuwa na kipaji kikubwa.

Kwa sasa dunia inamshuhudia Ronaldo aliye mahiri. Si kwamba amebadilika sana kiuchezaji, hapana, Ronaldo ni yule yule, isipokuwa maamuzi yake ya mwisho yanamfanya awe na rekodi bora uwanjani. Ama atafunga au kutoa pasi ya mwisho.

Kuna vitu vingi vinavyomfanya mwanasoka awe mahiri. Mashabiki wengi wa Tanzania tunawaangalia wanasoka wetu kijuujuu.

Mwanasoka mahiri ni yule mwenye matokeo uwanjani bila kujali kama ana kipaji kikubwa au hapana. Haijalishi kama una uwezo wa kupiga chenga uwanja mzima, kama huwezi kuisaidia timu kupata matokeo mazuri, huwezi kuwa mchezaji mahiri.

Mpaka wakati naandika makala hii, kwa mujibu wa takwimu za uwanjani, Ronaldo alikuwa mchezaji aliyepiga mashuti mengi zaidi katika lango la adui katika Ligi Kuu ya England. Alikuwa amepiga mashuti 90 yaliyolenga lango la adui.

Utaongeza nini kutoka kwake zaidi ya mabao yake 21 ya ligi yanayomfanya awe mchezaji wa nafasi ya kiungo wa pembeni aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England.

Amewaziba midomo mashabiki wengi wa soka ambao walikuwa wanamzomea katika viwanja vya soka na sehemu za kutazamia mechi za Ligi Kuu ya England.

Miaka kadhaa nyuma, Edibily Jonas Lunyamila alifanikiwa kuwa mmoja wa wachezaji wa aina hii. Achilia mbali uwezo wake wa kusisimua jukwaa, lakini alicheza mpira wa matokeo zaidi kuliko viungo wa pembeni wa sasa.

Halafu mtazame vizuri Cesc Fabregas. Huyu ni kiungo ambaye mashabiki wengi wa soka wanajikuta wakimtukuza bila ya kuchunguza ni kitu gani kinampa umaarufu.

Hana uwezo wa kupiga chenga maridadi na hata umbo lake mwenyewe halimruhusu. Si mpiga kanzu wala tobo, lakini ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, achilia mbali kufunga.

Kwa mujibu wa takwimu za uwanjani za Ligi Kuu ya England, Fabregas ndiye mchezaji pekee katika Ligi Kuu ya England anayeongoza kwa kupiga pasi nyingi zaidi. Kabla ya mechi ya leo dhidi ya Wigan Athletic, tayari amepiga pasi 1,676.

Kwa upande wa pasi za mwisho ambazo zilizaa mabao, amepiga 12, huku akiwa amezidiwa pasi mbili na kiungo wa pembeni wa Aston Villa, Ashley Young ambaye amepiga pasi 14.

Ukienda Uwanja wa Taifa utakutana na viungo wetu wengi ambao wengi tunawapa ‘vichwa’ kwa ajili ya mambo ya kipuuzi uwanjani, tobo, kanzu, na visigino ambavyo havizai mabao wala ‘move’ ya maana.

Kwa anachofanya kwa sasa nimeweza kukiona kwa wachezaji wachache sana katika miaka ya karibuni. Haruna Moshi na John Barasa ni miongoni mwa wachezaji ambao miaka ya karibuni waliweza kutuonyesha namna ya kupiga pasi za mwisho.

Lakini pia unaweza kumtazama mchezaji kama Javier Mascherano wa Liverpool. Huyu ni aina ya wachezaji wa kutazamwa uwanjani, kwa sababu katika soka la kisasa mashabiki wanajikita zaidi katika kushabikia wachezaji ambao ni rahisi kuyaona matokeo ya kazi zao.

Mara nyingi viungo wa ulinzi hawahesabiwi kama wachezaji hodari uwanjani na hata wakati wa usajili unapowadia, washambuliaji na viungo wanatazamwa kwa jicho la husuda zaidi.

Katika timu wachezaji wa aina yake ni muhimu mno. Unachoweza kujifunza kutoka kwa Mascherano ni uwezo wa kujitolea uwanjani kwa asilimia 100.

Ili uwe mchezaji kamili unapaswa ucheze kwa ajili ya timu. Ushinde kwa ajili ya timu, na moyo wako uwe umelazwa uwanjani kwa ajili ya timu.

Mpaka naandika makala hii, Mascherano alikuwa mchezaji aliyepora mipira mara nyingi zaidi katika ligi kuu ya England. Alikuwa amepora mipira mara 129.

Huwezi kupora mipira mingi uwanjani kwa bahati, unatakiwa kupigana na hasa katika Ligi Kuu ya England ambayo nayo washambuliaji na wachezaji wa nafasi ya kiungo ni wababe kama wachezaji wetu wa enzi za zamani.

Wakati umepita sasa kusifia wachezaji kihisia hisia. Kuna wachezaji wanapigiwa debe kila kukicha waitwe katika timu ya Taifa. Na wapo mashabiki wanaomtukana kocha wa timu ya taifa, Marcio Maximo pindi anapowaacha wachezaji fulani fulani.

Nadhani wakati umefika walau tuanze kutunza kumbukumbu zetu pindi tunapomshawishi kocha amchague au kumpanga mchezaji fulani katika timu ya taifa au klabuni.

Unapojaribu kumshawishi kocha amuite mchezaji fulani katika timu ya taifa, unaweza kujikumbusha kwamba amepiga pasi ngapi za mwisho na rekodi nyingine ndogo ndogo.

Bahati mbaya hata aina ya ushangiliaji wetu bado ni wa kizamani. Inawakilisha hisia zetu zinazowaelekeza wachezaji wetu wasifanye mambo ya maana uwanjani. Mchezaji anapiga chenga maridadi huku akielekea katika lango lake mwenyewe, inatusaidia nini?

Mchezaji anazunguka katikati ya uwanja na baadaye anatoa pasi ya kisigino kwa Nadir Cannavaro, jukwaa lake linalipuka kwa shangwe kubwa, inatusaidia nini?

Ukiutazama mchezo wa soka kwa sasa, kuna wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa lakini hawana msaada mkubwa katika timu. Na sasa makocha mbalimbali barani Ulaya wanajaribu kuepuka wachezaji wa namna hii.

Mchezaji kama Denilson wa Brazil alipewa kipaji kikubwa cha kumiliki mpira. Hata hivyo hakuwa na faida ya ushindi uwanjani na badala yake makocha wa Brazil wakamtumia kama mchezaji wa kupoteza muda uwanjani pindi timu inapokuwa inaongoza.

Na wapo makocha ambao wamekuwa wakiwachezesha wachezaji wengi ambao hawana vipaji vya soka, lakini wanaongoza kwa kutimiza majukumu yao uwanjani.

Tukianza kulitambua tatizo hili, wachezaji wengi chipukizi watajilea katika mazingira ya kuisaidia timu kwa njia mbalimbali na si kufurahisha majukwaa kama inavyotokea kwa wachezaji wengi wa zama hizi.

Lakini kwanza tuwaonyeshe rekodi hizi za akina Ronaldo, Mascherano na Fabregas. Tukizielewa na wenyewe wakazielewa, tutapata kizazi cha wanasoka wenye malengo uwanjani

No comments: