Saturday, 29 March 2008
Mhimili wa Arsenal uliotumika kuteketeza wazee wa AC Milan
Mhimili wa Arsenal uliotumika kuteketeza wazee wa AC Milan
ARSENAL kwa sasa imekuwa timu ya kwanza ya England kushinda kwenye Uwanja wa San Siro, baada ya kuibwaga AC Milan ya Italia kwa mabao 2-0, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita.
Alikuwa ni kiungo chipukizi mwenye umri wa miaka 20, Francesc Fabregas Soler au Cesc Fabregas kama alivyozoeleka mbele ya mashabiki, ambaye alikuwa wa kwanza kufungua ukurasa wa mabao kwa shuti la umbali wa mita 30.
Ama hakika mechi hiyo ilidhihirisha kupevuka kwa vijana au ‘Watoto wa Kocha Arsene Wenger’ na jambo la kufurahisha zaidi ni namna ambavyo Fabregas alicheza soka ya kiwango cha juu katika mechi hiyo ambayo imeifanya Arsenal kufuzu hatua ya Robo Fainali, baada ya sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza ambayo Arsenal ilikuwa mwenyeji.
Jambo jingine lililowafurahisha mashabiki wa Arsenal katika mechi hiyo ni namna Fabregas alivyocheza soka ya kuvutia kiasi cha kuwafunika wakongwe wa Milan, katika mechi ambayo ilitafsiriwa na wengi kuwa ni vita ya vijana na wazee wazoefu, akiwamo Paolo Maldini, anayeelekea umri wa miaka 40.
Wengi waliangalia namna wazoefu hao walivyochoshwa na watoto wa Wenger, hususan katika safu ya kiungo, ambako mwanasoka bora wa dunia, Ricardo Kaka alikuwa na wakati mgumu mbele ya Fabregas, ambaye kwa hakika katika mechi hiyo alimfunika, kwani ndiye aliyekuwa mchezaji nyota.
Ushindi huo umeacha swali moja kubwa, nalo ni je, Arsenal baada ya kuwabwaga mabingwa watetezi wa taji hilo, mabingwa ambao wana rekodi ya kulibeba taji hilo mara saba, wataweza kulibeba hapo Mei 21 katika mechi ya fainali huko Moscow, Urusi?
Hakuwa Fabregas pekee katika kundi hilo la watoto wa Wenger aliyefanya maajabu, bali nyota mwingine aliyewakuna wengi alikuwa ni chipukizi wa miaka 18, Theo Walcott, ambaye pasi yake murua ilitosha kuipa Arsenal bao la pili.
Walcott ambaye hivi karibuni alishutumiwa namna kasi ya kukua kwa soka yake ilivyo chini, alidhihirisha kwamba yuko makini, baada ya kuambaa na mpira na kupiga krosi safi ya chinichini iliyomkuta Emmanuel Adebayor, ambaye aliujaza mpira wavuni kiulaini.
Wakati mashabiki wakiendelea kusubiri mambo mazuri ya Walcott kadri siku zinavyozidi kwenda, gumzo kubwa kwa sasa ni kuhusu Fabregas, ambaye ni wazi amekuwa lulu na kiongozi wa chipukizi wenzake katika kuhakikisha wakongwe wa AC Milan wanaziaga fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Fabregas, aliyezaliwa Mei 4, 1987, Arenys de Mar, Hispania, ni mchezaji aliyeibukia katika klabu ya Barcelona akiwa kijana mdogo na hapana shaka klabu hiyo huenda inajuta kwa kumuacha aondoke, kwani kwa sasa ni lulu katika klabu ya Arsenal.
Wakati huo anakumbukwa zaidi namna alivyokuwa mahiri katika safu ya kiungo, lakini zaidi alikuwa ni kiungo mkabaji, ingawa mara kadhaa pia alionyesha umahiri katika kuzifumania nyavu kwa mabao yake safi na ya kuvutia na wakati mwingine alifunga mabao hata 30 kwa msimu mmoja.
Hofu ya kutopata nafasi ya kuitwa katika kikosi cha kwanza ilimuingia na hapo akaanza mipango ya kuihama Barcelona na ndipo alipotua rasmi Arsenal, Septemba 2003.
Siku zake za mwanzo zilikuwa ngumu katika jiji la London, hata hivyo urafiki wa karibu na mchezaji mwenzake, Philippe Senderos ulikuwa na msaada mkubwa kwa Fabregas, ambaye alizoea maisha na hata kuyafurahia.
Akiwa kijana wa miaka 16, Fabregas hakuwa na mawazo ya kupata nafasi katika kikosi cha kwanza mapema, alikuwa ni mwenye kuwaangalia wakongwe, Gilberto Silva na Patrick Vieira, wakati huo huo alikuwa makini katika mazoezi, huku akijifunza lugha ya Kiingereza.
Alicheza mechi yake ya kwanza mwezi mmoja baada ya kujiunga na timu hiyo, mechi ambayo ilikuwa ni ya Kombe la Ligi dhidi ya Rotherham United na hivyo kujiwekea rekodi ya kuwa mchezaji chipukizi mwenye umri mdogo kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Arsenal.
Katika mechi iliyofuata ambayo pia ilikuwa ni ya Kombe la Ligi, akiwa na miaka 16 na siku 177, Fabregas alikuwa chipukizi wa kwanza mwenye umri mdogo kufunga bao katika klabu ya Arsenal, ambayo katika mechi hiyo ilitoka na ushindi wa mabao 5–1 dhidi ya Wolves. Arsenal ilitwaa taji la Ligi Kuu msimu wa 2003/04, huku ikiwa na rekodi nzuri ya kutofungwa hata mechi moja, lakini Fabregas hakupewa medali ya ushindi huo kwa sababu hakucheza mechi hata moja ya ligi hiyo.
Mechi nyingine ya ushindani na ambayo inaweza kutajwa kuwa ya kujivunia katika siku za mwanzo mwanzo za Fabregas katika klabu ya Arsenal, ni ile ya kufungua msimu, mechi ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Manchester United, iliyochezwa mwanzoni mwa msimu wa 2004/05.
Hadi hapo tayari jina lake lilianza kuwa gumzo na aliwafurahisha wengi alipofunga bao wakati Arsenal ikiibugiza Blackburn mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya England na baada ya hapo aliendelea kuwa na namba, hususan alipoumia Vieira.
Balaa la majeruhi lilipoendelea kuiandama Arsenal kwa kuwakumba wachezaji wake, kina Edu na Gilberto Silva, Fabregas aliendelea kupata nafasi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hususan alipocheza Arsenal ilipoumana na Rosenborg na kuibuka na ushindi wa mabao 5–1 na yeye kufunga bao moja.
Fabregas aling’ara kwa mara nyingine na kujipatia taji lake la kwanza katika Kombe la FA, akiwa katika kikosi cha kwanza alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ambayo ilitwaa taji hilo kwa kuing’oa Man United kwa mikwaju ya penalti, hiyo ilikuwa ni mwaka 2005.
Kuondoka kwa Vieira ambaye alijiunga na Juventus ya Italia ilikuwa ni kufungua ukurasa mpya kwa Fabregas, ambaye alirithi jezi namba nne ya Vieira na akawa anashirikiana vyema na Gilberto katika safu ya kiungo, alicheza jumla ya mechi 49 katika msimu wa 2005/06 na licha ya kuwa na umri mdogo lakini kiwango chake cha uchezaji kilikuwa kivutio.
Wako waliohofia uwezo wake katika kumrithi Vieira, lakini mwenyewe baada ya kuaminiwa na Wenger alikuwa na staili yake ya kipekee ya kiuchezaji na wachambuzi wengi wa soka walifurahishwa na namna alivyocheza vizuri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus na Real Madrid.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya aliiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya fainali na kumana na klabu yake ya zamani ya Barcelona, mechi iliyochezwa Mei 2006, lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya Barcelona ambayo hatimaye ililibeba taji hilo, huku Arsenal ikimaliza msimu wa 2005/06 bila kombe.
Baada ya msimu huo, uvumi wa Fabregas kuihama Arsenal ulianza kuibuka, hususan Real Madrid ilielezea wazi wazi nia yake ya kutaka kumsajili kiungo huyo, lakini mwenyewe aliuzima uvumi huo Oktoba 2006, baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka sita na timu hiyo huku akidai kwamba anavutiwa na staili ya uchezaji ya Arsenal pamoja na imani kwa kocha wake Wenger.
Msimu wa 2006/07 ulikuwa ni wa mafanikio binafsi kwa Fabregas ambaye aliendelea kuwa nuru, alipata tuzo ya Golden Boy ya gazeti la michezo la Tutto Sport la Italia, alipata tuzo ya mwanasoka bora wa mwezi Januari 2007 wa Ligi Kuu ya England, pia alikuwamo katika timu bora ya mwaka 2006 ya UEFA pamoja na tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa Arsenal.
Kinachowafurahisha mashabiki wengi wa Arsenal kwa Fabregas si tuzo anazopata, bali ni aina yake ya uchezaji ambayo bila shaka ndiyo iliyomwezesha kupata umaarufu alionao sasa na hata kuwa gumzo duniani.
Ni kiungo ambaye wakati wote amekuwa muhimu na mwenye mchango katika kikosi cha kwanza cha Arsenal na pengine kilichotokea katika mechi na AC Milan ni sehemu tu ya mambo mazuri ambayo amekuwa akiyafanya.
Anaiongoza timu vizuri kuanzia safu ya kiungo, ni mbunifu mwenye mbinu za uhakika, anawapa wenzake pasi nzuri na wakati wote si mbinafsi anapokuwa na mpira, ni mahiri katika kupiga kona na jambo la mwisho ni namna anavyodhihirisha ukomavu wa soka lake, jambo ambalo kutokana na umri wake mdogo linaleta matumaini makubwa kwamba mambo mazuri kutoka kwake yataendelea kuonekana.
Kuna wakati aliwahi kulaumiwa na wachezaji wenzake kwa kutumia mbinu na akili zaidi kuliko nguvu, hata kufananishwa na bondia wa uzito mdogo, jambo ambalo ni wazi kwamba kwa sasa amejirekebisha, kwani kadri siku zilivyozidi kwenda amekuwa ni mchezaji wa kutumia nguvu.
Pamoja na umahiri na mafanikio yanayoonekana Arsenal, lakini katika timu ya Taifa ya Hispania, Fabregas bado hajafanya mambo makubwa, alianza kuichezea timu hiyo mwaka 2003 akiwa na timu ya vijana chini ya miaka 17 katika fainali za Kombe la Dunia nchini Finland.
Aliitwa katika timu ya wakubwa kwa mara ya kwanza mapema mwaka 2006 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ivory Coast na baada ya hapo ameendelea kuwa mchezaji muhimu wa timu hiyo na hata kuiwakilisha katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.
Huyo ndiye Francesc Fabregas Soler, mhimili muhimu wa Arsenal katika harakati za kutwaa taji la Ligi Kuu ya England na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment