Thursday, 27 March 2008
maximo na makocha wa yanga na simba
Maswali magumu zaidi katika soka ya Tanzania
kwanza. Katika siku za karibuni kumekuwa na rundo la makocha wa kigeni wanaotiririka katika klabu zetu kubwa zenye uwezo wa kuajiri makocha hawa wa bei ghali.
Wanashuka katika uwanja wa ndege pale Kipawa, wanapokewa kwa mbwembwe huku wakionekana kama vile ni malaika. Na ni wazi inaonekana kama vile wanabeba hatima ya klabu zetu ambazo wakati huo zinakuwa hazina makocha.
Ndiyo, na kwa sasa pia kuna rundo la wachezaji wa kigeni ambao wananunuliwa kwa bei ghali. Achana na wachezaji hawa wa kigeni, hata wachezaji wa nyumbani wananunuliwa kwa bei ghali na kila wanapotia saini katika klabu kubwa huwa wanasifiwa kuliko kiasi.
Kwa wageni, wengi wao pamoja na makocha wanalala katika hoteli za kifahari na wanalipwa fedha za kigeni kila mwisho wa mwezi unapowadia. Lakini tunaweza kujiuliza, mbona klabu zetu zimeendelea kukimbizana katika nyumba za wachawi zikijaribu kutafuta uchawi wa ushindi dhidi ya timu nyingine? Kawaulize waganga wa kienyeji watakwambia namna viongozi wa klabu kubwa wanavyopishana kwao kwa ajili ya kusaka ushindi.
Hapa ndipo tunapojiuliza; wachezaji hawa mahiri wa kigeni pamoja na makocha wa Kizungu, wana msaada gani kwa timu kama tuna imani kuwa mganga anaweza kusababisha tutoe kipigo kitakatifu kwa mtani wa jadi au timu pinzani ambayo tunacheza nayo?
Ukizubaa katika swali hili ambalo kamwe haliwezi kukupatia jibu yakinifu, utaumiza moyo wako bure. Kuna hili suala la waamuzi. Wanawindwa kuliko kiasi kwa ajili ya kuzipendelea timu fulani. Majina yao yanatafutwa mapema kabla hata ratiba haijatoka, baadaye wanatafutwa mitaani.
Ina maana gani ya kuleta wachezaji mahiri na kuingia gharama kubwa wakati tuna uwezo wa kumwona mwamuzi? Ina maana gani kumleta kocha wa Kizungu kwa mbwembwe kubwa kama akili yetu ya ushindi ipo kwa mwamuzi na mchawi?
Kwa nini gharama hizo zisitumike kumwongezea dau mganga ili tupate uhakika wa kutwaa ubingwa wa Afrika na makombe mengine ambayo yanakuja mbele yetu? Utaniambia kuwa uchawi hausaidii kama wachezaji hawapo fiti. Tunahitaji majaabu ya kushinda na ndio maana hatuna haja na habari za maslahi ya wachezaji. Inakuwaje mganga anatwambia wachezaji wawe fiti wakati hilo ni jukumu lake kutuwezesha kushinda?
Hatuna uhakika wa ufiti wa wachezaji na ndio maana tumekwenda kwake, iweje tuambiwe kuwa wachezaji wanahitaji kuwa fiti? Swali jingine gumu ni hili la kununua mechi kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani. Kama mmenunua waamuzi, mmekwenda kwa waganga, lakini pia mna wachezaji ambao wamewagharimu mamilioni ya fedha pamoja na makocha ambao mmewatoa mbali kwa ajili ya kufundisha mpira, ni kwa nini mkanunue wachezaji wa timu pinzani?
Tena timu pinzani ambayo msimu uliopita tuliinyong’onyesha kwa kwa kusajili wachezaji wake. Ina maana gani ya kuwa na wachezaji wazuri na kocha wa Kizungu kama bado tunanunua wapinzani? Si tungejaribu kuwa na timu ya kawaida na zile gharama za kununua wachezaji na kocha wa kigeni tukazipeleka kwa wachezaji wa timu pinzani ili tushinde mechi zote za ligi? Swali gumu!
Lakini pia tunajiuliza; kwa nini kama mmemalizana na mwamuzi mnalazimika kwenda kumalizana na mchawi? Ina maana hata mwamuzi anapaswa kulindwa na nguvu za kishirikina? Au kwa nini kama mmekwenda kwa mchawi bado mnakwenda tena kuonana na mwamuzi? Ina maana mwamuzi ana nguvu kuliko mchawi ambaye mmempatia Sh milioni 5 chini ya kivuli cha kamati ya ufundi?
Halafu inakuwaje mnaamini katika kila nguvu inayowazunguka? Mnaahidi Sh milioni 5 kwa kila mganga, Sh milioni 5 kwa mwamuzi na Sh milioni 1 kwa kila mchezaji kama mkishinda.
Na zaidi ya yote, mmetoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya wachezaji wa timu pinzani. Katika hao wote mnamwamini nani zaidi?
Ina maana timu ikishinda ni nani atakuwa ameleta ushindi klabuni? Mwamuzi, wachezaji, mchawi au wachezaji wa timu pinzani? Naamini itachukua miaka 100 kumwamini mtu ambaye atajigamba alisababisha timu ishinde.
Na hapo hapo tusisahau kuwa kocha naye atajigamba kuwa amepeleka ushindi klabuni. Atazungumza na vyombo vya habari kuwa wachezaji wamefuata maelekezo yake na ndiyo maana timu imeshinda. Ni nani atambishia?
Bahati mbaya hatuwezi kujibu maswali haya magumu na ndiyo maana tupo hapa tulipo. Kila siku tunamtafuta ‘mchawi’ kwa sababu hatujafahamu kuwa ni sisi wenyewe. Kwa maswali haya magumu ambayo hayawezi kujibika, tunapata taswira halisi ya ubabaishaji uliopo katika soka yetu
Hatuna programu za vijana kwa sababu tunaamini uchawi unaweza kusababisha tushinde mechi. Hatuamini katika soka ya vijana kwa sababu tunaamini kwamba mwamuzi anaweza akapelekea tushinde mechi.
Tunaamini katika soka ya wachezaji wa kigeni kwa sababu tumeshindwa kupata mwendelezo wa wachezaji wenye kaliba ya akina Sunday Manara. Na sasa tunaishi kwa imani zaidi badala ya kufuata misingi halisi ya soka. Kama hatuwezi kujijibu maswali haya magumu tuliyojiuliza, ukweli unabaki pale pale kwamba soka ni mchezo wa sayansi. Hakuna uchawi wala habari ya mwamuzi.
Kama kuna ubishi katika hili basi tuialike Timu ya Taifa ya Brazil tumwone mganga au mwamuzi atakayezuia kipigo dhidi yetu.
Tuondokane na ubabaishaji katika ngazi za chini hadi juu. Hizi si zama za kumwona mwamuzi wala kumtafuta mchawi. Mambo haya tunaweza kuyafanya kwa kujidanganya katika soka yetu ya ndani, lakini katika ngazi za kimataifa tutashindwa.
Waghana walishindwa katika ardhi yao, na kila siku tunaziona timu nyingi ambazo zinashindwa katika ardhi zao. Hata hivyo wenzetu walifanikiwa kujibu maswali haya magumu na ndio maana kila wanaposhindwa wanatafuta mbinu zaidi za kusonga mbele.
Ni lazima tupate swali moja tu; la kwa nini wachezaji wetu hawachezi vizuri uwanjani? Haya ya wachawi, kununua wachezaji wa timu pinzani, kununua waamuzi yamepitwa na wakati na ndiyo ambayo yametubakisha hapa tulipo. Inachekesha sana. Na nadhani ni wakati wa kujibu maswali haya magumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment