Thursday, 27 March 2008
maisha ya critiano ronaldo
cristiano :Kinda la Ferguson linalowachungulia Kaka na Ronaldinho Ulaya champion
Klabu ya kwanza kuichezea akiwa kinda ni SL Benfica ambapo baadaye alijiunga na mpinza mkubwa wa timu hiyo, Sporting. Hata hivyo hakudumu kwa muda mrefu, kwani alijiunga na klabu ya Andorinha, ambayo baba yake mzazi alikuwa ni mshirika mkubwa tangu akiwa na umri wa miaka minane.
Mwaka 1995, jina la Ronaldo lilikuwa kubwa nchini Ureno hususan mjini Madeira alipozaliwa, hali hiyo ilisababisha timu mbili za eneo hilo, CS Maritimo na CD Nacional kupigana vikumbo zikitaka kunasa dole gumba lake.
Hata hivyo, timu ya Nacional ndiyo iliyofanikiwa kumnasa mchezaji huyo, lakini baadaye alirejea kuichezea Klabu ya Sporting ambapo alijiunga na kikosi cha Yosso.
Kutokana na uwezo wake kuimarika, alichaguliwa kuichezea Timu ya Taifa ya Ureno katika michuano ya UEFA chini ya umri wa miaka 17 (U-17), kiwango alichokionesha kwenye kitimtim hicho kilimuweka roho juu aliyekuwa Kocha wa Liverpool FC, Gerard Houllier.
Hata hivyo, Houllier alisitisha juhudi za kumnasa kinda huyo kwa madai kwamba umri wake wa miaka 16 aliokuwa nao wakati huo ungemchukua muda mrefu kukomaa kisoka.
Kipigo cha mabao 3-1, Manchester United ilichokipata katika Uwanja wa Lisbon nchini Ureno kutoka kwa Sporting, huku Ronaldo akiwa anawika katika winga ya kulia, kilimtoa Sir Alex Ferguson udenda, ambaye kipindi hicho alikuwa na mikakati ya kutafuta winga Yosso wa kulia.
Majira ya joto, Ferguson alifanikiwa kunasa dole gumba la kinda huyo kwa Pauni za Uingereza milioni 12 ambapo alimpa mikoba ya David Beckham aliyekuwa amehamia Real Madrid ya Hispania.
Ronaldo alikabidhiwa jezi namba saba ambayo inaheshimika Man United, kutokana na kuvaliwa na nyoto muhimu waliowahi kuwika katika klabu hiyo kama George Best, Bryan Robson, Eric Cantona na David Beckham, hiyo ilikuwa kama njozi mpya kwa kinda huyo, kwani awali akiwa Sporting alikuwa akitumia jezi namba 28.
Kama ulivyo mfumo wa Man United kwa washambuliaji wake kucheza kwa kubadilishana namba wawapo uwanjani, Ronaldo amemudu vema utaratibu huo kwani siyo ajabu kumuona akicheza winga ya kulia, mshambuliaji wa kati ama namba kumi.
Oktoba 29, 2005, Ronaldo aliifungia Manchester United goli la 1000 katika Ligi Kuu ya nchini humo maarufu kama ‘Barclays Premiership’, wakati timu hiyo ilipoikandamiza Middlesbrough kwa mabao 4-1.
Desemba 2006, Ronaldo aliwika na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Man United, baada ya kuifungia magoli sita katika mechi tatu alizoshuka dimbani.
Julai 8, 2006, wakati Ureno ikicheza na England kwenye robo fainali za kombe la dunia, Wayne Rooney alimtupia lawama Ronaldo kuwa alimshawishi mwamuzi kumtoa nje kwa kadi nyekundu baada ya Rooney kumchezea vibaya, Ricardo
Carvalho.
Kitendo hicho kiliibua mambo mengi kwa wachezaji hao kwani magazeti ya nchini England, The Sun na The Daily Mirror yalichapisha habari kuwa, kutolewa kwa Rooney kuliigharimu timu yao kusukumizwa nje kwenye michuano hiyo kama ilivyokuwa kwa David Beckham mwaka 1998 katika kinyang’anyiro kama hicho.
Suala hilo lilimpandisha mzuka Rooney na kuweka wazi kwamba, Ronaldo atakapokanyaga ardhi ya England kuitumikia Klabu yake ya Man United, atamfanyia kitu mbaya.
Kinda huyo wa Kireno alijibu mapigo kwa kusema kwamba atahamia Real Madrid ya Hispania, hata hivyo Ferguson alimtumia msaidizi wake Carlos Queiroz kuweza kuzungumza na Ronaldo ambapo naye aliweza kuongea na Rooney na hivyo wawili hao wakaelewana.
Suala hilo liliifanya Man United, ilipofika Aprili 13 mwaka 2007, kumsahwishi mchezaji huyo kufunga ndoa ya muda mrefu na klabu hiyo, ambapo alikubali kusaini mkataba mpya utakaomuwezesha kulipwa Pauni 120,000 kwa wiki.
Kitita hicho kinamfanya kuwa wa kwanza kupokea dau kubwa katika historia ya Klabu ya Mashetani Wekundu hao, baada ya kuanguka dole gumba hilo alisema “Ninajisikia furaha kubwa kuwepo katika klabu hii, ninachotaka kwa sasa ni kushinda vikombe zaidi, natumaini hilo litawezekana msimu huu”.
Katika mechi za kimataifa hususan wakati akiichezea timu yake ya taifa Ronaldo aliweza kuifungia Ureno bao la kufutia machozi dhidi ya Ugiriki wakati ilipofungwa mabao 2-1 katika ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 2004.
Kadhalika aliweza kuifungia Ureno bao la kwanza katika nusu fainali hizo dhidi ya Uholanzi, wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Ronaldo pia aliiwakilisha Ureno katika michuano ya Olimpiki kipindi cha majira ya joto mwaka, 2004, pia alishika nafasi ya pili ya ufungaji bora katika kinyang’anyiro cha kuwania kufuzu kombe la dunia katika ukanda wa Ulaya baada ya kucheka na nyavu mara saba.
Bao lake la kwanza kufunga katika michuano ya kombe la dunia lilikuwa la penaliti dhidi ya Iran.
Februari 6, 2007, yaani ikiwa ni siku moja baada ya kusheherekea siku ya kuzaliwa kwake, Scolari alimtangaza Ronaldo kuwa nahodha wa Ureno katika mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil.
Baada ya kumpa unahodha, Scolari alisema alifanya hivyo kutokana na maagizo aliyopewa na Rais wa Chama cha Soka nchini humo (PFF), Carlos Silva ambaye alifariki dunia siku mbili kabla.
Ronaldo yupo katika mtihani mgumu wa kuwabwaga wachezaji wengine wawili wa Kibrazil Ricardo Izecson dos Santos Leite ‘Kaka’ na Ronaldinho Gaucho ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuweza kuibuka mwanasoka bora wa FIFA msimu huu.
Vikombe alivyoshinda akiwa na Manchester United
Ubingwa wa England: 2006-2007
Kombe la FA : 2004
Kombe la Ligi: 2006
Ngao ya jamii: 2007
Jina kamili Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro
Kuzaliwa Februari 5, 1985 (miaka 22)
Alipozaliwa Funchal, Madeira, Ureno
Urefu 1.85 m
Nafasi Mshambuliaji wa pembeni, Kulia
Klabu Manchester United
Jezi namba 7
Timu ya taifa Ureno kuanzia 2003
Makala haya yameandaliwa na ISAAC KIJOTI kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa.
Dear Guest you have enter our site without being Registered. We recommend to register to view more...
"Mgeni wetu unatakiwa Kuregista kupata Udaku Wote..."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment