Saturday, 29 March 2008

mwameja

Mkapa, Mohammed Hussein walichemsha Simba tulipoilamba Yanga 4-1 mwaka 1994


MOHAMED MWAMEJA:

“Tulipoingia kipindi cha pili tuliendelea kuwashambulia Yanga na nakumbuka katika dakika ya 76 hivi, Simba tulifanya shambulizi moja kali langoni mwa timu ya Yanga na kufanikiwa kupata bao la tatu. Bao letu hilo lilifungwa na Madaraka Selemani

TIMU ya Simba ya Dar es Salaam kwa miaka mingi iliyopita imebahatika kuwa na makipa mahiri ambao waliweza kutamba ndani na hata nje ya nchi.

Katika miaka ya 1990, mmoja wa makipa ambaye klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam ilibahatika kumpata si mwingine, bali ni Mohamed Mwameja.

Mwameja kabla ya kujiunga na Simba alivuma sana akiwa na timu za Ndovu ya Arusha na Coastal Union ya Tanga.

Kutokana na umahiri wake mkubwa katika namba yake hiyo, haikuchukua muda mrefu akiwa na klabu ya Simba alichaguliwa kujiunga na timu ya Taifa (Taifa Stars).

Kutokana na uwezo aliokuwa nao wa kulinda lango lake vizuri, wapenzi wa soka walimbatiza jina la Tanzania One, ikiwa na maana kuwa ndiye kipa namba moja wa Tanzania au timu ya Taifa.

Sifa aliyokuwa nayo nyingine ni udakaji wa mipira ya penalti ambayo ilimpatia sifa kubwa hapa nchini pamoja na Afrika Mashariki na Kati.

Hivi karibuni gazeti la DIMBA lilifanya mahojiano naye kuhusu mechi anayoikumbuka vizuri wakati wa enzi zake za kucheza soka ya ushindani.

Katika mahojiano hayo anasema pamoja na kucheza mechi nyingi wakati anacheza soka ya ushindani, lakini kuna mechi moja ambayo anaikumbuka vizuri mpaka leo hii.

Mechi hiyo ni wakati alipokuwa na timu yake ya Simba walipocheza na wapinzani wao wa jadi, Yanga. Anasema mechi hiyo ilikuwa ni ngumu na yenye upinzani mkali, kwa sababu kila timu ilikuwa inataka kuibuka mshindi.

"Simba tuliipania sana mechi hiyo kwa sababu mechi ya mwisho tulipocheza na Yanga walitufunga mabao 2-0 katika mzunguko wa kwanza.

“Nakumbuka mechi hiyo ilichezwa siku ya Jumamosi, Julai 2, mwaka 1994 katika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na ilikuwa ni mashindano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu) na matokeo yalikuwa ni mazuri kwetu Simba, kwani tuliwafunga Yanga mabao 4-1.

“Mchezo ulianza taratibu, huku kila timu ikiusoma mchezo wa mwenzake. Pamoja na kuanza taratibu lakini ni sisi Simba ambao tulikuwa tunapeleka mashambulizi mengi langoni mwa timu ya Yanga.

“Nakumbuka katika dakika ya 10 hivi, Simba tulifanya shambulizi moja la nguvu langoni mwa timu ya Yanga na kufanikiwa kupata bao lililofungwa na Athumani China, lakini mwamuzi Bakari Mtangi alilikataa bao hilo na kusema kuwa China alikuwa ameotea.

“Baada ya kushambulia kwa kipindi kirefu kidogo katika dakika ya 16 hivi hatimaye Simba tulifanikiwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na George Masatu kwa mpira wa adhabu.

“Bao hilo lilipatikana baada ya Nico Bambaga kumfanyia madhambi mshambuliaji wetu Edward Chumila.

“Haukupita muda mrefu Yanga nao walifanya shambulizi moja la nguvu langoni kwetu na kufanikiwa kusawazisha. Bao lao lilifungwa na mlinzi wao aliyecheza vizuri siku hiyo, Costantino Kimanda kwa mpira wa adhabu ndogo.

“Baada ya Simba kufungwa bao hilo, tuliendelea kuwashambulia Yanga na katika dakika ya 34 hivi ya kipindi hicho cha kwanza tulifanikiwa kupata bao la pili.

“Bao hilo lilifungwa na Athumani China kwa mpira wa kona iliyopigwa na George Masatu.

“Nakumbuka katika kipindi hicho cha kwanza Yanga walimpumzisha Kenneth Mkapa na nafasi yake kuchukuliwa na Willy Martin. Pia walimtoa Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Yusuf ‘Tigana’.

“Mpaka tunakwenda mapumziko Simba tulikuwa mbele kwa mabao 2-1.

“Tulipoingia kipindi cha pili tuliendelea kuwashambulia Yanga na nakumbuka katika dakika ya 76 hivi, Simba tulifanya shambulizi moja kali langoni mwa timu ya Yanga na kufanikiwa kupata bao la tatu. Bao letu hilo lilifungwa na Madaraka Selemani.

“Pia nakumbuka katika kipindi hicho cha pili mwamuzi wa mchezo huo, Bakari Mtangi alimtoa nje ya uwanja mlinzi Willy Martin wa Yanga kwa kumpiga kichwa cha nyuma mshambuliaji wetu Dua Said.

“Baada ya kuwafunga Yanga mabao matatu tuliendelea kuwashambulia Yanga na walionekana kuzidiwa kabisa na mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na washambuliaji wetu.

“Nakumbuka katika dakika za mwisho mwisho wakati tukiendelea kuwashambulia, tulifanikiwa kupata bao la nne baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu ya Yanga.

“Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Simba tulitoka uwanjani tukiwa wababe kwa kuwafunga Yanga mabao 4-1.

“Ninaikumbuka mechi hiyo kwa sababu mbili, kwanza ilikuwa ni mechi ngumu na yenye ushindani mkubwa sana. Wachezaji wa Simba kabla ya kucheza mechi hiyo tulikuwa na ‘tension’ kubwa na kudhani kuwa hatuwezi kuwafunga Yanga.

“Pili ninaikumbuka mechi hiyo kwa sababu mechi ya mwisho kucheza na Yanga Simba tulifungwa mabao 2-0, hivyo na sisi tulilipa kisasi kwa kuwafunga mabao 4-1.

“Nakumbuka kikosi chetu Simba kilichocheza na Yanga kilikuwa ni mimi, Godwin Aswile, Deo Mkuki, Mustapha Hoza, George Masatu, Iddi Seleman, Athumani China, Hussein Masha/George Lucas, Madaraka Seleman, Edward Chumila (sasa marehemu) na Dua Said.

“Kikosi cha Yanga kilichocheza siku hiyo kilikuwa, Stephen Nemes, Seleman Mkati, Kenneth Mkapa/Willy Martin, Salum Kabunda, Costantino Kimanda, Nico Bambaga, Mohamed Hussein/Ally Yusuf ‘Tigana’, Sekilojo Chambua, Said Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu), James Tungaraza na Edibily Lunyamila.

“Hiyo ndiyo mechi ninayoikumbuka vizuri sana mpaka leo hii na ambayo siwezi kuisahau maishani mwangu.”

Maelezo haya yamechukuliwa na Henry Paul mjini Dar es Salaam.

Wasifu Wake:
Jina: Mohamed Mwameja
Umri: Miaka 44
Mchezo: Soka
Nafasi: Golikipa
Timu: Makidile (Tanga), Bandari (Tanga), Ndovu (Arusha), Coastal Union na
Taifa Stars.
Kazi: Biashara.

No comments: